Hizi ndizo Aya za Biblia zinazozungumzia mfalme Daudi
2 Samweli 7 : 4 – 29
4 Ikawa usiku uo huo, neno la BWANA likamfikia Nathani kusema,
5 Nenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, BWANA asema hivi, Je! Wewe utanijengea nyumba, nikae ndani yake?
6 Kwa maana mimi sikukaa ndani ya nyumba, tangu siku ile niliyowatoa wana wa Israeli katika Misri, hata leo, lakini nimekaa katika hema na maskani.
7 Mahali kote nilikokwenda na wana wa Israeli wote, je! Nimesema neno lolote na mtu yeyote wa waamuzi wa Israeli, niliyemwagiza kuwalisha watu wangu Israeli, nikisema, Mbona hamkunijengea nyumba ya mierezi?
8 Basi, sasa, mwambie mtumishi wangu, Daudi, maneno haya, BWANA wa majeshi asema hivi, Nilikutwaa katika zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo, ili uwe mkuu juu ya watu wangu, juu ya Israeli;
9 nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina kuu, kama jina la wakuu walioko duniani.
10 Tena nitawaagizia mahali watu wangu Israeli, nami nitawapanda, wapate kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa tena, kama hapo kwanza;
11 naam, kama ilivyokuwa tangu siku ile nilipowaamuru waamuzi, wawe juu ya watu wangu Israeli; nami nitakustarehesha mbele ya adui zako wote. Tena BWANA anakuambia ya kwamba BWANA atakujengea nyumba.
12 Nawe siku zako zitakapotimia, ukalala na baba zako, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayetoka viunoni mwako, nami nitauimarisha ufalme wake.
13 Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha ufalme wake nitakiimarisha milele.
14 Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; akitenda maovu nitamwadhibu kwa fimbo ya binadamu na kwa mapigo ya wanadamu;
15 lakini fadhili zangu hazitamwondoka, kama vile nilivyomwondolea Sauli, niliyemwondoa mbele yako.
16 Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitaimarishwa milele.
17 Kwa maneno hayo yote, na kwa maono hayo yote, ndivyo Nathani alivyonena na Daudi.
18 Ndipo Daudi, mfalme, akaingia, akaketi mbele za BWANA, akasema, Mimi ni nani, Bwana MUNGU, na nyumba yangu ni nini, hata umenileta hadi hapa?
19 Tena jambo hili lilikuwa dogo machoni pako, Ee Bwana MUNGU; hata umeleta habari ya nyumba yangu mimi, mtumishi wako, kwa miaka mingi inayokuja baadaye; na hayo kwa namna ya kibinadamu, Ee Bwana MUNGU.
20 Na mimi, Daudi, nikuambie nini tena zaidi? Iwapo wewe umemjua mtumishi wako, Ee Bwana MUNGU.
21 Kwa ajili ya neno lako, na kwa moyo wako mwenyewe, umetenda makuu hayo yote, ili umjulishe mtumishi wako.
22 Kwa hiyo, wewe ndiwe mkuu, Ee BWANA Mungu, kwa maana hakuna kama wewe, wala hapana Mungu mwingine ila wewe, kwa kadiri tulivyosikia kwa masikio yetu.
23 Tena ni taifa lipi duniani lililo kama watu wako, kama Israeli, ambalo Mungu alikwenda kuwakomboa kwa ajili yake, wawe watu wake mwenyewe, akajifanyie jina, na kutenda mambo makuu kwa ajili yenu, na mambo ya kuogofya kwa ajili ya nchi yako, mbele ya watu wako, uliowakomboa kutoka Misri wawe wako, kutoka katika mataifa na miungu yao.
24 Nawe ulijifanyia imara watu wako wa Israeli, wawe watu wako milele; nawe, BWANA, umekuwa Mungu wao.
25 Basi sasa, Ee BWANA Mungu, neno lile ulilolinena kuhusu mtumishi wako, na kuhusu nyumba yangu, uliimarishe milele, ukatende kama ulivyosema.
26 Jina lako na litukuzwe milele, kwa kusema, BWANA wa majeshi ndiye Mungu juu ya Israeli; na nyumba ya mtumishi wako, Daudi, itaimarika mbele zako.
27 Kwa kuwa wewe, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli umenifunulia mimi, mtumishi wako, ukisema, Nitakujengea nyumba; kwa hiyo mimi, mtumishi wako, nimepata ujasiri nikuombe ombi hili.
28 Na sasa, Ee Bwana MUNGU, wewe ndiwe Mungu, na maneno yako ndiyo kweli, nawe umemwahidia mtumishi wako jambo hili jema
29 basi, sasa, uwe radhi, ukaibariki nyumba ya mtumishi wako, ipate kudumu milele mbele zako; kwa maana wewe, Ee Bwana MUNGU, umelinena na kwa baraka yako nyumba ya mtumishi wako na ibarikiwe milele.
1 Wafalme 1 : 1 – 53
1 Mfalme Daudi alikuwa mzee, mkongwe katika siku zake, nao wakamfunika nguo, lakini asipate joto.
2 Kwa hiyo watumishi wake wakamwambia, Bwana wangu mfalme na atafutiwe kijana mwanamwali; naye asimame mbele ya mfalme, amtunze; alale kifuani mwako, ili bwana wangu mfalme apate joto
3 Basi wakatafuta msichana mzuri katika nchi yote ya Israeli, wakamwona Abishagi, Mshunami, wakamleta kwa mfalme.
4 Naye msichana huyo alikuwa mzuri sana; akamtunza mfalme, akamtumikia; lakini mfalme hakumjua.
5 Ndipo Adonia mwana wa Hagithi akatakabari, akasema, Mimi nitakuwa mfalme. Akajiwekea tayari magari na wapanda farasi, na watu hamsini wapige mbio mbele yake.
6 Tena baba yake hakumchukiza wakati wowote kwa kusema, Mbona umefanya hivi? Kisha, alikuwa mtu mzuri sana; naye alizaliwa baada ya Absalomu.
7 Akashauriana na Yoabu, mwana wa Seruya, na Abiathari, kuhani; nao wakamsaidia Adonia, wakamfuata.
8 Ila Sadoki, kuhani, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Nathani, nabii, na Shimei, na Rei, na mashujaa wa Daudi, hao hawakuwa pamoja na Adonia.
9 Adonia akatoa sadaka ya kondoo, ng’ombe na ndama wanono, karibu na jiwe la Zohelethi, lililo karibu na chemchemi Enrogeli; akawaita ndugu zake wote, wana wa mfalme, na watu wote wa Yuda, watumishi wa mfalme;
10 ila nabii Nathani, Benaya, walinzi wa mfalme na Sulemani ndugu yake hakuwaalika.
11 Ndipo Nathani akamwambia Bathsheba, mamaye Sulemani, akasema, Je! Hukusikia ya kuwa Adonia, mwana wa Hagithi, amekuwa mfalme, na bwana wetu Daudi hana habari?
12 Haya basi, nikupe shauri, tafadhali, upate kuiokoa roho yako, na roho ya mwanao Sulemani.
13 Nenda uingie ndani kwa mfalme Daudi, ukamwambie, Je! Hukuniapia mimi mjakazi wako, Ee mfalme, bwana wangu, kusema, Hakika yake Sulemani mwana wako atamiliki baada yangu, na kuketi katika kiti changu cha enzi? Mbona basi anamiliki Adonia?
14 Tazama, wakati ule utakapokuwa katika kusema na mfalme, mimi nami nitaingia nyuma yako, na kuyahakikisha maneno yako.
15 Basi Bathsheba akaingia ndani kwa mfalme, ndani ya chumba chake; naye mfalme alikuwa mzee sana; na Abishagi, Mshunami, alikuwa akimtumikia mfalme.
16 Bathsheba akainama, akamsujudia mfalme. Naye mfalme akamwuliza, Wataka nini?
17 Akamwambia, Bwana wangu, uliniapia mimi mjakazi wako kwa BWANA, Mungu wako, ya kwamba, bila shaka Sulemani mwanao atamiliki baada yangu, yeye ndiye atakayeketi katika kiti changu cha enzi.
18 Na sasa, angalia, Adonia anamiliki; na wewe, bwana wangu mfalme, huna habari.
19 Tena amechinja ng’ombe, na vinono, na kondoo tele, na kuwaita wana wa mfalme wote pia, na Abiathari, kuhani, na Yoabu, jemadari wa jeshi. Ila Sulemani, mtumishi wako, huyu hakumwita.
20 Ee mfalme, bwana wangu, macho ya Israeli wote yanakuelekea wewe, kwamba uwaambie ni nani atakayeketi katika kiti chako cha enzi baada yako, Ee mfalme, bwana wangu.
21 Ama sivyo itakuwa, bwana wangu mfalme atakapolala pamoja na baba zake, mimi na mwanangu Sulemani tutahesabiwa kuwa wahalifu.
22 Basi tazama, alipokuwa katika kusema na mfalme, Nathani, nabii, aliingia.
23 Wakamwambia mfalme wakasema, Tazama, Nathani, nabii. Naye alipoingia ndani mbele ya mfalme, akamsujudia kifudifudi.
24 Nathani akasema, Ee mfalme, bwana wangu, je! Wewe umesema ya kwamba, Adonia atamiliki baada yangu, ndiye atakayeketi katika kiti changu cha enzi?
25 Maana leo ameshuka, na kuchinja ng’ombe, na vinono, na kondoo tele, naye amewaita wana wote wa mfalme, na majemadari wa jeshi, na Abiathari, kuhani; na tazama, wanakula na kunywa mbele yake, wakisema, Na aishi mfalme Adonia!
26 Lakini mimi, mtumishi wako, na Sadoki, kuhani, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Sulemani, mtumishi wako, hakutuita sisi.
27 Je! Bwana wangu mfalme ndiye aliyelitenda jambo hili, bila kutujulisha sisi watumishi wako ni nani atakayeketi katika kiti cha enzi cha bwana wangu mfalme baada yake?
28 Ndipo mfalme Daudi akajibu, akasema, Niitieni Bathsheba. Basi akaingia ndani kwa mfalme, akasimama mbele ya mfalme.
29 Naye mfalme akaapa, akasema, BWANA aishivyo, aliyenikomboa roho yangu katika shida zote,
30 hakika yake nitafanya leo kama vile nilivyokuapia kwa BWANA, Mungu wa Israeli, nikasema, Kwa yakini Sulemani mwanao atamiliki baada yangu, naye ndiye atakayeketi katika kiti changu cha enzi badala yangu.
31 Ndipo Bathsheba akainama kifudifudi, akamsujudia mfalme, akasema, Bwana wangu mfalme Daudi na aishi milele.
32 Naye mfalme Daudi akasema, Niitie Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na Benaya, mwana wa Yehoyada. Nao wakaingia ndani mbele ya mfalme.
33 Naye mfalme akawaambia, Twaeni pamoja nanyi watumishi wa bwana wenu, mkampandishe Sulemani mwanangu juu ya nyumbu wangu mimi mkamteremshe mpaka Gihoni;
34 kisha Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na wamtie mafuta huko, awe mfalme juu ya Israeli; kapigeni panda, mkaseme, Mfalme Sulemani na aishi!
35 Kisha pandeni juu nyuma yake, naye atakuja ili aketi katika kiti changu cha enzi; kwa maana atakuwa mfalme badala yangu; ndiye niliyemweka awamiliki Israeli na Yuda.
36 Basi Benaya, mwana wa Yehoyada, akamjibu mfalme, akasema, Amina; BWANA, Mungu na bwana wangu mfalme, na aseme vivyo hivyo.
37 Kama vile BWANA alivyokuwa pamoja na bwana wangu mfalme, kadhalika na awe pamoja na Sulemani, na kufanya kiti chake cha enzi kuwa kitukufu kuliko kiti cha enzi cha bwana wangu mfalme Daudi.
38 Basi wakashuka Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Wakerethi, na Wapelethi, wakampandisha Sulemani juu ya nyumbu wa mfalme Daudi, wakampeleka mpaka Gihoni.
39 Na Sadoki, kuhani, akatwaa ile pembe ya mafuta katika Hema, akamtia Sulemani mafuta. Nao wakapiga panda; na watu wote wakasema, Na aishi Mfalme Sulemani!
40 Kisha watu wote wakapanda juu nyuma yake, watu wakapiga mazomari, wakafurahi kwa shangwe kuu mno, hata nchi ikapasuka kwa sauti zao.
41 Basi Adonia, na wageni wote waliokuwa pamoja naye, wakasikia hayo walipokuwa wamekwisha kula. Naye Yoabu aliposikia sauti ya panda alisema, Za nini kelele hizi za mji uliotaharuki?
42 Naye alipokuwa katika kunena, tazama Yonathani, mwana wa Abiathari kuhani, akafika. Naye Adonia akasema, Karibu; maana wewe u mtu mwema, unaleta habari njema.
43 Naye Yonathani akajibu, akamwambia Adonia, Hakika bwana wetu mfalme Daudi amemtawaza Sulemani.
44 Tena mfalme alipeleka pamoja naye Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Wakerethi, na Wapelethi, wakampandisha juu ya nyumbu wa mfalme.
45 Kisha Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, wakamtia mafuta huko Gihoni, ili awe mfalme. Nao wamepanda juu kutoka huko wakifurahi, hata mji ukavuma. Ndizo kelele zile mlizozisikia.
46 Na tena, Sulemani ameketi katika kiti cha enzi cha ufalme.
47 Na tena, watumishi wa mfalme walifika, ili wambariki bwana wetu mfalme Daudi, wakisema, Mungu wako na alikuze jina la Sulemani kuliko jina lako, na kukifanya kiti chake cha enzi kuwa kitukufu kuliko kiti chako. Naye mfalme akainama chini juu ya kitanda chake.
48 Na tena, mfalme akasema hivi, BWANA, Mungu wa Israeli, ahimidiwe, aliyenipa leo hivi mtu wa kuketi katika kiti changu cha enzi, nayo macho yangu yakiwa yanaona hayo.
49 Ndipo wageni wote waliokuwa pamoja na Adonia wakaogopa, wakaondoka, wakaenda zao kila mtu njia yake.
50 Adonia naye akaogopa mbele ya Sulemani; akaondoka, akaenda, akazishika pembe za madhabahu.
51 Akaambiwa Sulemani, kusema, Tazama, Adonia amwogopa mfalme Sulemani; kwani, tazama, amezishika pembe za madhabahu, akisema, Mfalme Sulemani na aniapie leo kwamba hataniua mimi mtumwa wake kwa upanga.
52 ① Sulemani Akasema, Akionekana kuwa mtu wa kweli, hata unywele wake mmoja hautaanguka chini; lakini uovu ukionekana ndani yake, atakufa.
53 Basi mfalme Sulemani akatuma watu, wakamteremsha toka madhabahuni. Naye akaja, akamwinamia mfalme Sulemani; naye Sulemani akamwambia, Nenda nyumbani kwako.
Yohana 14 : 26
26 Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.
2 Samweli 12 : 1 – 31
1 Ndipo BWANA akamtuma Nathani aende kwa Daudi. Naye akamwendea, akamwambia, Palikuwa na watu wawili katika mji mmoja; mmoja wao alikuwa tajiri, wa pili maskini.
2 Yule tajiri alikuwa na kondoo na ng’ombe wengi sana;
3 bali yule maskini hakuwa na kitu, ila mwana-kondoo mmoja, mdogo, ambaye amemnunua na kumlea; naye akakua pamoja naye, na pamoja na wanawe; hula sehemu ya posho lake, na kukinywea kikombe chake, na kulala kifuani mwake, akawa kwake kama binti.
4 Kisha msafiri mmoja akamfikia yule tajiri, naye akaacha kutwaa mmoja wa kondoo zake mwenyewe au mmoja wa ng’ombe zake mwenyewe, ili kumwandalia yule msafiri aliyemfikia, bali alimnyang’anya yule maskini mwana-kondoo wake, akamwandalia yule mtu aliyemfikia.
5 Ndipo hasira ya Daudi ikawaka sana juu ya mtu yule; akamwambia Nathani, Aishivyo BWANA, mtu huyo aliyetenda jambo hili, hakika yake astahili kufa;
6 naye atamrudishia yule mwana-kondoo mara nne, kwa sababu ametenda neno hili, na kwa sababu hakuwa na huruma.
7 Basi Nathani akamwambia Daudi, Wewe ndiwe mtu huyo. BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nilikutia mafuta, uwe mfalme juu ya Israeli, nikakuokoa kutoka kwa mkono wa Sauli;
8 nami nikakupa nyumba ya bwana wako, na wake za bwana wako kifuani mwako; nikakupa nyumba ya Israeli na ya Yuda; na kama hayo yangalikuwa machache, ningalikuongezea mambo mengine mengi.
9 Kwa nini umelidharau neno la BWANA, na kufanya yaliyo mabaya machoni pake? Umempiga Uria, Mhiti, kwa upanga, nawe umemtwaa mkewe awe mke wako, nawe umemwua huyo kwa upanga wa Waamoni.
10 Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako.
11 BWANA asema hivi, Angalia, nitakuzushia uovu katika nyumba yako, nami nitawatwaa wake zako mbele ya macho yako, na kumpa jirani yako, naye atalala na wake zako hadharani.
12 Maana wewe ulifanya jambo lile kwa siri; bali mimi nitalifanya jambo hili mbele ya Israeli wote na hadharani.
13 ① Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia BWANA dhambi. Nathani akamwambia Daudi, BWANA naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa.
14 ② Lakini, kwa kuwa kwa tendo hili umewapa adui za BWANA nafasi kubwa ya kukufuru, mtoto atakayezaliwa kwako hakika atakufa.
15 ③ Naye Nathani akaondoka kwenda nyumbani kwake. Basi BWANA akampiga yule mtoto ambaye mkewe Uria alimzalia Daudi naye akawa mgonjwa sana.
16 ④ Basi Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya mtoto; Daudi akafunga, akaingia, akalala chini usiku kucha.
17 Nao wazee wa nyumba yake wakaondoka, wakasimama karibu naye, ili wamwinue kutoka chini; lakini hakukubali, wala hakula chakula pamoja nao.
18 Ikawa siku ya saba, yule mtoto akafa. Nao watumishi wa Daudi wakaogopa kumwambia ya kuwa mtoto amekufa, maana, walisema, Angalieni, yule mtoto alipokuwa angali hai, tulisema naye, asitusikilize sauti zetu; si atajidhuru, tukimwambia ya kuwa mtoto amekufa?
19 Lakini alipoona ya kuwa watumishi wake wananong’onezana, Daudi alitambua ya kuwa mtoto amekufa; basi Daudi akawauliza watumishi wake, Je! Mtoto amekufa? Nao wakasema, Amekufa.
20 ⑤ Ndipo Daudi akainuka pale chini akaoga, akajipaka mafuta, akabadili mavazi yake; akaingia nyumbani mwa BWANA, akasali; kisha akaenda nyumbani kwake, na alipotaka wakamwandalia chakula, naye akala.
21 Watumishi wake wakamwambia, Ni jambo gani hili ulilolitenda? Ulifunga na kulia kwa ajili ya mtoto, alipokuwa hai; lakini mtoto alipokuwa amekufa, uliinuka ukala chakula.
22 ⑥ Akasema, Mtoto alipokuwa hai, nilifunga, nikalia; kwa maana nilisema, Ni nani ajuaye kama BWANA atanihurumia, mtoto apate kuishi?
23 ⑦ Lakini sasa amekufa nifungie nini? Je! Naweza kumrudisha tena? Mimi nitakwenda kwake lakini yeye hatanirudia mimi.
24 ⑧ Naye Daudi akamfariji Bathsheba mkewe, akaingia kwake, akalala naye; naye akazaa mwana, akamwita jina lake Sulemani. Naye BWANA akampenda;
25 akapeleka kwa mkono wa Nathani, nabii, naye akamwita jina lake Yedidia,[9] kwa ajili ya BWANA.
26 ⑩ Yoabu akapigana juu mji wa Waamoni, akautwaa mji wa kifalme.
27 Yoabu akatuma wajumbe waende kwa Daudi, kusema Nimeshindana na Raba, hata nimeutwaa huo mji wa maji.
28 Basi sasa kusanya watu waliobaki, ukauzunguke mji, na kuutwaa; nisije mimi nikautwaa mji, ukaitwe jina langu.
29 Basi Daudi akawakusanya watu wote akaenda Raba, akapigana nao, akautwaa.
30 ⑪ Kisha akamnyang’anya mfalme wao taji toka kichwani pake; na uzani wake ulikuwa talanta ya dhahabu, nalo lilikuwa na vito vya thamani ndani yake; akavikwa Daudi kichwani. Akazitoa nyara za huo mji, nyingi sana.
31 Naye akawatoa watu waliokuwamo, akawaweka kwenye kazi ya[10] misumeno, na sululu za chuma, na mashoka ya chuma, akawafanyiza kazi tanurini mwa matofali; ndivyo alivyoifanya miji yote ya wana wa Amoni. Kisha Daudi akarudi na watu wote Yerusalemu.
Zaburi 144 : 1
1 ② Na ahimidiwe BWANA, mwamba wangu, Aifundishaye mikono yangu vita, Na vidole vyangu kupigana.
Zaburi 46 : 1
1 Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.
Leave a Reply