Hizi ndizo Aya za Biblia zinazozungumzia kuungama dhambi
Yakobo 5 : 16
16 Basi ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, ili mpate kuponywa. Sala yake mwenye haki ina nguvu nyingi, na hutenda mengi.
1 Yohana 1 : 9
9 Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kututakasa na udhalimu wote.
1 Timotheo 2 : 5
5 Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu;
Zaburi 32 : 5
5 Ndipo nikakuungamia dhambi yangu, Wala sikuuficha upotovu wangu. Nilisema, Nitayakiri maasi yangu kwa BWANA, Nawe ukanisamehe upotovu wa dhambi yangu.
Yohana 20 : 23
23 Na wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.
2 Samweli 12 : 13
13 ① Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia BWANA dhambi. Nathani akamwambia Daudi, BWANA naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa.
Zaburi 51 : 1 – 19
1 Ee Mungu, unirehemu, kulingana na fadhili zako. Kiasi cha wingi wa rehema zako, Uyafute makosa yangu.
2 Unioshe kabisa uovu wangu, Unitakase dhambi zangu.
3 ① Maana nimejua mimi makosa yangu Na dhambi yangu iko mbele yangu daima.
4 ② Nimekutenda dhambi Wewe peke yako, Na kufanya maovu mbele za macho yako. Wewe ujulikane kuwa una haki unenapo, Na kuwa safi utoapo hukumu.
5 ③ Tazama, nikazaliwa nikiwa na hatia; Mama yangu akanichukua mimba nikiwa na dhambi.
6 Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni; Nawe utanifundisha hekima kwa siri,
7 Unisafishe kwa hisopo nami nitakuwa safi, Unioshe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji.
8 Unifanye kusikia furaha na shangwe, Mifupa uliyoiponda ifurahi.
9 Usitiri uso wako usitazame dhambi zangu; Uzifute hatia zangu zote.
10 ④ Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya na kuithibiti roho yangu.
11 ⑤ Usinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu usiniondolee.
12 ⑥ Unirudishie furaha ya wokovu wako; Unitegemeze kwa roho ya upendo.
13 Nitawafundisha wakosaji njia zako, Na wenye dhambi watarejea kwako.
14 Ee MUNGU, Mungu wa wokovu wangu, Uniponye na umwagaji wa damu, Na ulimi wangu utaiimba haki yako.
15 Ee Bwana, uifumbue midomo yangu, Na kinywa changu kitazinena sifa zako.
16 Maana hupendezwi na dhabihu, na kama ningeitoa, Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa.
17 Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika; Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau.
18 Uitendee mema Sayuni kwa radhi yako, Uzijenge kuta za Yerusalemu.
19 ⑦ Ndipo utakapopendezwa na dhabihu za haki, Na sadaka za kuteketezwa, na kafara. Ndipo watakapotoa ng’ombe Juu ya madhabahu yako.
1 Yohana 2 : 1
1 Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki,
Mathayo 9 : 6 – 8
6 Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (amwambia yule mwenye kupooza) Inuka, ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwako.
7 Akaondoka, akaenda zake nyumbani kwake.
8 Makutano walipomwona, walishikwa na hofu, wakamtukuza Mungu, aliyewapa watu amri ya namna hii.
Yohana 20 : 19 – 24
19 Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu.
20 Naye akiisha kusema hayo, akawaonesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana.
21 Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawatuma ninyi.
22 Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu.
23 Na wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.
24 ① Lakini mmoja wa wale Kumi na Wawili, Tomaso, aitwaye Pacha, hakuwako pamoja nao alipokuja Yesu.
Matendo 19 : 18
18 Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao.
Waraka kwa Waebrania 4 : 16
16 Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.
Waraka kwa Waebrania 10 : 10
10 Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.
Warumi 7 : 15 – 25
15 ⑫ Maana sijui nifanyalo, kwa sababu lile nilipendalo, silitendi; bali lile nilichukialo ndilo ninalolitenda.
16 Lakini kama nikilitenda lile nisilolipenda, naikiri ile sheria ya kuwa ni njema.
17 Basi sasa si mimi nafsi yangu ninayetenda hilo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu
18 ⑬ Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema; kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema siwezi.
19 Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo.
20 Basi kama lile nisilolipenda ndilo nilitendalo, si mimi nafsi yangu nilitendaye, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.
21 Basi nimeona sheria hii, ya kuwa kwangu mimi nitakaye kutenda lililo jema, lipo lililo baya.
22 Kwa maana naifurahia sheria ya Mungu kwa utu wa ndani,
23 ⑭ lakini katika viungo vyangu naona sheria iliyo mbali, inapiga vita na ile sheria ya akili zangu, na kunifanya mateka wa ile sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu.
24 Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?
25 ⑮ Namshukuru Mungu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu. Basi, kama ni hivyo, mimi mwenyewe kwa akili zangu naitumikia sheria ya Mungu, bali kwa mwili wangu sheria ya dhambi.
2 Wakorintho 5 : 18
18 Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho;
1 Petro 2 : 9
9 ⑦ Bali ninyi ni uzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu;
Ufunuo 1 : 6
6 na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina.
Leave a Reply