Hizi ndizo Aya za Biblia zinazozungumzia dua
Wafilipi 4 : 6
6 Msijisumbue kwa neno lolote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.
Wafilipi 4 : 6 – 7
6 Msijisumbue kwa neno lolote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.
7 Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.
Mathayo 6 : 9 – 13
9 Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje,
10 Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.
11 Utupe leo riziki yetu.
12 Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu.
13 Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. [Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.]
Yakobo 5 : 16
16 Basi ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, ili mpate kuponywa. Sala yake mwenye haki ina nguvu nyingi, na hutenda mengi.
1 Petro 5 : 7
7 ⑱ huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.
Waraka kwa Waebrania 4 : 16
16 Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.
Mathayo 6 : 6
6 Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.
Danieli 9 : 1 – 27
1 Katika mwaka wa kwanza wa Dario, mwana wa Ahasuero, wa uzao wa Wamedi, aliyetawazwa kuwa mfalme juu ya milki ya Wakaldayo;
2 katika mwaka wa kwanza wa kutawala kwake, mimi Danieli, kwa kuvisoma vitabu, nilifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la BWANA lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini.
3 Nikamwelekezea Bwana Mungu uso wangu, ili kusihi kwa maombi, na dua, pamoja na kufunga, na kuvaa nguo za magunia na majivu.
4 Nikamwomba BWANA, Mungu wangu, nikaungama, nikasema, Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake;
5 tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako;
6 wala hatukuwasikiliza watumishi wako, manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, na watu wote wa nchi.
7 Ee Bwana, haki ina wewe, lakini kwetu sisi kuna aibu, kama hivi leo; kwa watu wa Yuda, na kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa Israeli wote, walio karibu na hao walio mbali, katika nchi zote ulikowafukuza, kwa sababu ya makosa yao waliyokukosa.
8 Ee Bwana, kwetu sisi kuna aibu, kwa wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, kwa sababu tumekutenda dhambi.
9 Rehema na msamaha ni kwa Bwana Mungu wetu, ingawa tumemwasi;
10 wala hatukuitii sauti ya BWANA, Mungu wetu, kwa kwenda katika sheria zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa cha watumishi wake, manabii.
11 Naam, Israeli wote wameivunja sheria yako, kwa kugeuka upande, wasiisikilize sauti yako; basi kwa hiyo laana imemwagwa juu yetu, na kiapo kile kilioandikwa katika Sheria ya Musa, mtumishi wa Mungu; kwa sababu tumemtenda dhambi.
12 Naye ameyathibitisha maneno yake, aliyoyanena juu yetu, na juu ya waamuzi wetu waliotuamua, kwa kumletea mambo maovu makuu; maana chini ya mbingu zote halikutendeka jambo kama hili, lilivyotendeka juu ya Yerusalemu.
13 Kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Musa, mabaya haya yote yametupata lakini hata hivyo hatukumwomba BWANA, Mungu wetu, atupe fadhili zake, ili tugeuke na kuyaacha maovu yetu, na kuitambua kweli yake.
14 Basi BWANA anayachungulia mabaya hayo, akatuletea; maana BWANA, Mungu wetu ni mwenye haki katika kazi zake zote azitendazo; na sisi hatukuitii sauti yake.
15 Na sasa, Ee Bwana Mungu wetu, uliyewatoa watu wako hawa katika nchi ya Misri kwa mkono hodari, ukajipatia sifa, kama ilivyo leo; tumefanya dhambi, tumetenda maovu.
16 Ee Bwana sawasawa na haki yako yote, nakusihi, hasira yako na ghadhabu yako zigeuzwe na kuuacha mji wako Yerusalemu, mlima wako mtakatifu; maana kwa sababu ya dhambi zetu, na maovu ya baba zetu, Yerusalemu na watu wako wamepata kulaumiwa na watu wote wanaotuzunguka.
17 Basi sasa, Ee Mungu wetu, yasikilize maombi ya mtumishi wako, na dua zake, ukaangazishe uso wako juu ya patakatifu pako palipo ukiwa, kwa ajili ya Bwana.
18 Ee Mungu wangu, tega sikio lako, ukasikie; fumbua macho yako ukautazame ukiwa wetu, na mji ule ulioitwa kwa jina lako; maana hatukutolei maombi yetu kwa sababu ya haki yetu, lakini kwa sababu ya rehema zako nyingi.
19 Ee Bwana, usikie; Ee Bwana, usamehe; Ee Bwana, usikilize, ukatende, usikawie; kwa ajili yako wewe, Ee Mungu wangu; kwa sababu mji wako na watu wako wanaitwa kwa jina lako.
20 Basi hapo nilipokuwa nikisema, na kuomba, na kuiungama dhambi yangu, na dhambi ya watu wangu Israeli, na kuomba dua yangu mbele za BWANA, Mungu wangu, kwa ajili ya mlima mtakatifu wa Mungu wangu;
21 naam, nilipokuwa nikinena katika kuomba, mtu yule, Gabrieli, niliyemwona katika njozi hapo kwanza, akirushwa upesi, alinigusa panapo wakati wa dhabihu ya jioni.
22 Akaniagiza, akaongea nami, akasema, Ee Danieli, nimetokea sasa, ili nikupe akili upate kufahamu.
23 Mwanzo wa maombi yako ilitolewa amri, nami nimekuja kukupasha habari; maana wewe unapendwa sana; basi itafakari habari hii, na kuyafahamu maono haya.
24 Muda wa majuma sabini umeamriwa juu ya watu wako, na juu ya mji wako mtakatifu, ili kukomesha makosa, na kumaliza dhambi, na kufanya upatanisho kwa ajili ya uovu, na kuleta haki ya milele, na kutia mhuri maono na unabii, na kumtia mafuta yeye aliye mtakatifu.
25 Basi ujue na kufahamu, ya kuwa tangu kuwekwa amri ya kutengeneza na kuujenga upya Yerusalemu hata zamani zake masihi aliye mkuu; kutakuwa na majuma saba; na katika majuma sitini na mawili utajengwa tena pamoja na njia kuu zake na handaki, naam, katika nyakati za taabu.
26 Na baada ya yale majuma sitini na mawili, masihi atakatiliwa mbali, naye atakuwa hana kitu; na watu wa mkuu atakayekuja watauangamiza mji, na patakatifu; na mwisho wake utakuwa pamoja na gharika, na hata mwisho ule vita vitakuwapo; ukiwa umekwisha kukusudiwa.
27 ① Naye atafanya agano thabiti na watu wengi kwa muda wa juma moja; na kwa nusu ya juma hiyo ataikomesha sadaka na dhabihu; na mahali pake litasimama chukizo la uharibifu; na hivyo, hata ukomo, na ghadhabu iliyokusudiwa imemwagwa juu yake mwenye kuharibu.
Zaburi 91 : 1 – 16
1 Aketiye mahali pa siri pake Aliye Juu Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi.
2 Atasema, BWANA ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini.
3 Maana Yeye atakuokoa kutoka kwa mtego wa mwindaji, Na katika maradhi mabaya.
4 ⑳ Kwa manyoya yake atakufunika, Chini ya mbawa zake utapata kimbilio; Uaminifu wake ni ngao na kigao.
5 Hutaogopa hatari za usiku, Wala mshale urukao mchana,
6 Wala mapigo yajayo usiku, Wala maafa yatokeayo adhuhuri,
7 Hata watu elfu wakianguka ubavuni pako. Naam, watu elfu kumi katika mkono wako wa kulia! Wewe hutakaribiwa na maafa.
8 Ila kwa macho yako utatazama, Na kuyaona malipo ya wasio haki.
9 Kwa kuwa Wewe BWANA ndiwe kimbilio langu; Umemfanya Aliye Juu kuwa makao yako.
10 Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako.
11 Kwa kuwa atakuagizia malaika wake Wakulinde katika njia zako zote.
12 Mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.
13 Utawakanyaga simba na nyoka, Mwanasimba na joka utawakanyaga kwa miguu.
14 Kwa kuwa amekaza kunipenda Nitamwokoa; na kumweka palipo juu, Kwa kuwa amenijua Jina langu.
15 Ataniita nami nitamwitikia; Nitakuwa pamoja naye taabuni, Nitamwokoa na kumtukuza;
16 Kwa siku nyingi nitamshibisha, Nami nitamwonesha wokovu wangu.
1 Wathesalonike 5 : 17
17 ombeni bila kukoma;
Yakobo 5 : 13
13 Kuna mtu miongoni mwenu anayeteseka? Na aombe. Ana moyo wa kuchangamka? Na aimbe zaburi.
Zaburi 20 : 4 – 5
4 Akujalie kwa kadiri ya haja ya moyo wako, Na kukutimizia mipango yako yote.
5 Na tuushangilie wokovu wako, Kwa jina la Mungu wetu tuzitweke bendera zetu. BWANA akutimizie matakwa yako yote.
Mathayo 26 : 41
41 ⑰ Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho iko radhi, lakini mwili ni dhaifu.
Luka 18 : 1
1 ⑫ Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa.
Wagalatia 3 : 14
14 ili kwamba baraka ya Abrahamu iwafikie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani.
Wafilipi 4 : 19
19 Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu.
Kumbukumbu la Torati 28 : 1 – 68
1 ⑳ Itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani;
2 na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya BWANA, Mungu wako.
3 Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani.
4 Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, kuongezeka kwa ng’ombe wako, na wadogo wa kondoo wako.
5 Litabarikiwa kapu lako, na chombo chako cha kukandia unga.
6 Utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa na utokapo.
7 BWANA atawafanya adui zako wainukao juu yako kupigwa mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba.
8 BWANA ataiamuru baraka ije juu yako katika ghala zako, na mambo yote utakayotia mkono wako; naye atakubarikia katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako.
9 BWANA atakuweka uwe taifa takatifu kwake, kama alivyokuapia; utakaposhika maagizo ya BWANA, Mungu wako, na kutembea katika njia zake.
10 Na mataifa yote ya duniani watakuona umeitwa kwa jina la BWANA, nao watakuwa na hofu kwako.
11 BWANA atakufanya uwe na wingi wa uheri, katika uzao wa tumbo lako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, na uzao wa nchi yako, katika nchi BWANA aliyowaapia baba zako kwamba atakupa.
12 Atakufunulia BWANA hazina yake nzuri, nayo ni mbingu, kwa kutoa mvua ya nchi yako kwa wakati wake, na kwa kubarikia kazi yote ya mkono wako; nawe utakopesha mataifa mengi, wala hutakopa wewe.
13 BWANA atakufanya kuwa kichwa, wala si mkia; nawe utakuwa juu tu, wala huwi chini; utakapoyasikiza maagizo ya BWANA, Mungu wako, nikuagizayo hivi leo, kuyaangalia na kufanya;
14 msipokengeuka katika maneno niwaamuruyo leo kwa lolote, kwenda mkono wa kulia wala wa kushoto, kwa kuifuata miungu mingine na kuitumikia.
15 Lakini itakuwa usipotaka kuisikiza sauti ya BWANA, Mungu wako, usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na amri zake, nikuagizazo hivi leo, ndipo zitakapokujia laana hizi zote na kukupata.
16 Utalaaniwa mjini, utalaaniwa na mashambani.
17 Litalaaniwa kapu lako na chombo chako cha kukandia.
18 Utalaaniwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, kuongezeka kwa ng’ombe wako, na wadogo wa kondoo wako.
19 Utalaaniwa uingiapo, utalaaniwa na utokapo,
20 BWANA atakuletea laana na mashaka, na kukemewa, katika yote utakayotia mkono wako kuyafanya, hata uangamie na kupotea kwa upesi; kwa ule uovu wa matendo yako, uliyoniacha kwayo.
21 BWANA atakuambatanisha na tauni, hata atakapokwisha kukuondoa katika nchi uingiayo kwa kuimiliki.
22 BWANA atakupiga kwa kifua kikuu, na kwa homa, na kwa kuwashwa, na kwa joto jingi, na kwa upanga, na kwa ukaufu, na kwa koga; navyo vitakufukuza hata uangamie.
23 Na mbingu zako zilizo juu ya kichwa chako zitakuwa shaba, na nchi iliyo chini yako itakuwa chuma.
24 BWANA atafanya mvua ya nchi yako iwe vumbi na mchanga; itakujilia juu yako kutoka mbinguni hata uangamie.
25 BWANA atakufanya upigwe mbele ya adui zako; utawatokea juu yao kwa njia moja, lakini utakimbia mbele yao kwa njia saba; nawe utatupwa huku na huko katika falme zote za duniani.
26 Na mzoga wako utakuwa chakula cha ndege wote wa angani, na wanyama wote wa duniani, pasiwe na mtu wa kuwafukuza.
27 BWANA atakupiga kwa majipu ya Misri, na kwa bawasiri, na kwa pele, na kwa kujikuna, ambayo hupati kupoa.
28 BWANA atakupiga kwa wazimu, na kwa upofu, na kwa bumbuazi la moyoni;
29 utakwenda kwa kupapasapapasa mchana, kama apapasavyo kipofu gizani, wala hufanikiwi katika njia zako; nawe sikuzote utaonewa na kutekwa nyara, wala hapatakuwa na mtu wa kukuokoa.
30 Utaposa mke na mume mwingine atalala naye; utajenga nyumba usiikae; utapanda mizabibu usitumie matunda yake.
31 Ng’ombe wako atachinjwa mbele ya macho yako, usile nyama yake; utanyang’anywa punda wako mbele ya uso wako kwa jeuri, usirudishiwe; kondoo wako watapewa adui zako, usipate mtu wa kukuokoa.
32 Wanao na binti zako litapewa taifa lingine, na macho yako yataangalia, na kuzimia kwa kuwatamani mchana kutwa; wala hapatakuwa na kitu katika uwezo wa mkono wako.
33 Matunda ya nchi yako, na taabu yako yote, vitaliwa na taifa usilolijua; utaonewa tu, na kupondwa chini daima;
34 hata uwe mwenye wazimu kwa yaonwayo na macho yako, utakayoyaona.
35 BWANA atakupiga magoti na miguu kwa jipu lililo zito, usilopata kupozwa, tokea wayo wa mguu mpaka utosi wa kichwa.
36 BWANA atakupeleka wewe, na mfalme wako utakayemweka juu yako, kwa taifa usilolijua wewe wala baba zako; nawe huko utatumikia miungu mingine ya miti na mawe.
37 Nawe utakuwa ushangao, na mithali, na dharau, kati ya mataifa yote huko atakakokuongoza BWANA.
38 Mbegu nyingi utazichukua nje shambani, lakini utavuna haba, kwa kuwa nzige watazila.
39 Utapanda mizabibu na kuitengeza, wala hutakunywa katika divai yake, wala kuichuma kwani italiwa na mabuu.
40 Utakuwa na mizeituni katika mipaka yako yote usijipake mafuta yake; kwa kuwa mzeituni wako utapukutika.
41 Utazaa wana na binti, lakini hawatakuwa wako wewe; kwa sababu watakwenda utumwani.
42 Miti yako yote, na mazao ya nchi yako, nzige watakuwa nayo.
43 Mgeni aliye kati yako atazidi kupaa juu yako; nawe utazidi kushuka chini.
44 Yeye atakukopesha, wala wewe usimkopeshe; yeye atakuwa ni kichwa, wewe utakuwa mkia.
45 Na laana hizi zote zitakujilia juu yako, zitakuandama na kukupata, hata uangamizwe, kwa kuwa hukuisikiza sauti ya BWANA, Mungu wako, kushika maagizo yake na amri zake alizokuagiza;
46 nazo zitakuwa juu yako kwa ishara na ajabu, na juu ya uzao wako milele;
47 ① kwa kuwa hukumtumikia BWANA, Mungu wako, kwa furaha na moyo wa kushukuru, kwa ajili ya ule wingi wa vitu vyote;
48 ② kwa hiyo utawatumikia adui zako atakaowaleta BWANA juu yako, kwa njaa, na kwa kiu, na kwa uchi, na kwa uhitaji wa vitu vyote; naye atakuvika kongwa la chuma shingoni mwako, hata atakapokwisha kukuangamiza.
49 ③ BWANA atakuletea taifa juu yako kutoka mbali, kutoka ncha ya dunia, kama arukavyo tai; taifa usiloufahamu ulimi wake;
50 ④ taifa lenye uso mkali, ambalo haliangalii uso wa mzee, wala halipendelei kijana;
51 ⑤ naye atakula uzao wa ng’ombe wako wa mifugo, na uzao wa nchi yako mpaka utakapokwisha kuangamizwa; wala hatakuachia nafaka, wala divai, wala mafuta, wala kuongezeka kwa ng’ombe wako, wala wana-kondoo wako, hata atakapokwisha kukuangamiza.
52 ⑥ Naye atakuhusuru katika malango yako yote, hata kuta zako ndefu, zenye maboma, ulizokuwa ukiziamini, zishuke, katika nchi yako yote kila upande; naye atakuhusuru katika malango yako yote kila upande, katika nchi yako yote aliyokupa BWANA, Mungu wako.
53 ⑦ Nawe utakula uzao wa tumbo lako mwenyewe, nyama ya wana wako na binti zako aliokupa BWANA, Mungu wako; katika mazingirwa na katika mkazo utakaokazwa na adui zako.
54 Mtu mume kati yenu aliye mwororo na laini sana, jicho lake litakuwa ovu juu ya nduguye, na juu ya mke wa kifuani mwake, na juu ya masalio ya wanawe waliosalia naye;
55 hata asitake wao mmojawapo apewe katika nyama ya wanawe atakaowala, kwa kuwa hana kitu kilichomsalia kwake; katika mazingirwa na mkazo utakaokazwa na adui yako katika malango yako yote.
56 Mwanamke kati yenu aliye mwororo na laini, ambaye hangehatarisha kuweka wayo wa mguu wake nchi kwa umalidadi na ulaini, jicho lake huyu litakuwa ovu juu ya mume wa kifuani mwake, na juu ya mwanawe, na juu ya binti yake,
57 ⑧ na juu ya mchanga wake atokaye katikati ya miguu yake, na juu ya wanawe atakaowazaa; kwa kuwa atawala kwa siri, kwa uhitaji wa vitu vyote; katika mazingirwa na mkazo utakaokazwa na adui yako katika malango yako.
58 ⑩ Kama hutaki kutunza kufanya maneno yote ya torati hii yaliyoandikwa katika kitabu hiki, upate kulicha jina hili la fahari na utisho, BWANA, MUNGU WAKO;
59 ⑪ ndipo atakapofanya BWANA mapigo yako yawe ya ajabu, na mapigo ya uzao wako, mapigo makubwa kwa kweli, ya kudumu sana, na magonjwa mazito ya kudumu sana.
60 Naye atakurejezea maradhi yote ya Misri juu yako uliyokuwa ukiyaogopa, nayo yataambatana nawe.
61 Tena kila ugonjwa, na kila pigo yasiyoandikwa katika kitabu cha Torati hii, atakutia nayo BWANA juu yako, hata utakapokwisha kuangamizwa.
62 ⑫ Nanyi mtasalia wachache kwa hesabu, ninyi mliokuwa mfano wa nyota za mbinguni kwa wingi; kwa kuwa hukuisikiza sauti ya BWANA, Mungu wako.
63 ⑬ Tena itakuwa, kama vile alivyokuwa akifurahi BWANA juu yenu kwa kuwatendea mema na kuwafanya kuwa wengi, ndivyo atakavyofurahi BWANA juu yenu kwa kuwapoteza na kuwaangamiza; nanyi mtanyakuliwa katika hiyo nchi mwingiayo kuimiliki.
64 ⑭ BWANA atakutawanya katika mataifa yote, tokea ncha hii ya dunia hata ncha hii ya dunia; nawe huko utatumikia miungu mingine usiyoijua wewe wala baba zako, nayo ni miti na mawe.
65 ⑮ Wala katika mataifa hayo hutapata raha iwayo yote, wala hutakuwa na kituo cha wayo wa mguu wako; lakini BWANA atakupa huko moyo wa kutetema, na macho ya kuzimia, na roho ya kudhoofika;
66 na uzima wako utakuwa na wasiwasi mbele yako; nawe utakuwa na woga usiku na mchana, wala hutaamini kamwe maisha yako;
67 ⑯ asubuhi utasema, Laiti ingekuwa jioni! Na jioni utasema, Laiti ingekuwa asubuhi! Kwa kicho cha moyo wako utakavyokucha, na kuona kwa macho yako utakavyoona.
68 ⑰ BWANA atakurudisha tena Misri kwa merikebu, kwa njia ambayo nilikuambia, Hutaiona tena popote; nanyi huko mtajiuza nafsi zenu kwa adui zenu kuwa watumwa na wajakazi, wala hapana atakayewanunua.
Waefeso 5 : 20
20 na kumshukuru Mungu Baba sikuzote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo.
1 Timotheo 2 : 8
8 Basi, nataka wanaume waombe kila mahali, huku wakiinua mikono iliyotakata pasipo hasira wala majadiliano.
2 Wakorintho 4 : 16
16 Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku.
Leave a Reply