Hizi ndizo Aya za Biblia zinazozungumzia ndoa
1 Wakorintho 7 : 1 – 40
1 Basi kuhusu mambo yale mliyoandika, ni heri mwanamume asimguse mwanamke.
2 Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe.
3 Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake.
4 Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe.
5 Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkarudiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu.
6 Lakini nasema hayo, kwa kutoa idhini yangu, si kwa amri.
7 Ila nipendalo ni kwamba watu wote wawe kama mimi nilivyo; lakini kila mtu ana karama yake mwenyewe itokayo kwa Mungu, huyu hivi, na huyu hivi.
8 Lakini nawaambia wale wasiooa bado, na wajane, Ni heri wakae kama mimi nilivyo.
9 Lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe; maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa.
10 Lakini wale waliokwisha kuoana nawaagiza; wala hapo si mimi, ila Bwana; mke asiachane na mumewe;
11 lakini, ikiwa ameachana naye, na akae asiolewe, au apatane na mumewe; tena mume asimwache mkewe.
12 Lakini watu wengine nawaambia mimi, wala si Bwana, ya kwamba iwapo ndugu mmoja ana mke asiyeamini, na mke huyo anakubali kukaa naye asimwache.
13 Na mwanamke, ambaye ana mume asiyeamini, na mume huyo anakubali kukaa naye, asimwache mumewe.
14 Kwa maana yule mume asiyeamini hutakaswa katika mkewe; na yule mke asiyeamini hutakaswa katika mumewe; kama isingekuwa hivyo, watoto wenu wangekuwa si safi; bali sasa ni watakatifu.
15 Lakini yule asiyeamini akiondoka, na aondoke. Hapo huyo ndugu mume au ndugu mke hafungiki. Lakini Mungu ametuita katika amani.
16 Kwa maana wajuaje, wewe mwanamke, kama utamwokoa mumeo? Au wajuaje, wewe mwanamume, kama utamwokoa mkeo?
17 Lakini kama Bwana alivyomgawia kila mtu, kama Mungu alivyomwita kila mtu, na aende vivyo hivyo. Ndivyo ninavyoagiza katika makanisa yote.
18 Je! Mtu fulani ameitwa akiwa amekwisha kutahiriwa? Asijifanye kana kwamba hakutahiriwa. Mtu fulani ameitwa akiwa hajatahiriwa bado? Basi asitahiriwe.
19 Kutahiriwa si kitu, na kutotahiriwa si kitu bali kuzihifadhi amri za Mungu.
20 Kila mtu na akae katika hali ile ile ambayo alikuwa nayo alipoitwa.
21 Je! Uliitwa u mtumwa? Usione ni vibaya lakini kama ukiweza kuwa na uhuru, afadhali kuutumia.
22 Kwa maana yeye aliyeitwa katika Bwana hali ya utumwa, ni huru wa Bwana. Vivyo hivyo yeye naye aliyeitwa hali ya uhuru, ni mtumwa wa Kristo.
23 Mlinunuliwa kwa thamani; msiwe watumwa wa wanadamu.
24 Ndugu zangu, kila mtu na akae mbele za Mungu katika hali iyo hiyo aliyoitwa nayo.
25 Kuhusu wanawali sina amri ya Bwana, lakini natoa shauri langu, mimi niliyejaliwa kwa rehema za Bwana kuwa mwaminifu.
26 Basi, naona hili kuwa jema, kwa ajili ya shida iliyopo, kwamba ni vema mtu akae kama alivyo.
27 Je! Umefungwa kwa mke? Usitake kufunguliwa. Umefunguliwa? Usitafute mke.
28 Lakini, kama ukioa, huna hatia; wala mwanamwali akiolewa, hana hatia; lakini watu kama hao watakuwa na dhiki katika mwili nami nataka kuwazuilia hayo.
29 Lakini, ndugu, nasema hivi, muda ubakio si mwingi; basi tokea sasa wale walio na wake na wawe kama hawana;
30 na wale waliao kama hawalii; na wale wafurahio kama hawafurahi; na wale wanunuao, kama hawana kitu.
31 Na wale wautumiao ulimwengu huu, kama hawautumii sana; kwa maana mambo ya ulimwengu huu yanapita.
32 Lakini nataka msiwe na masumbufu. Yeye asiyeoa hujishughulisha na mambo ya Bwana, ampendezeje Bwana;
33 bali yeye aliyeoa hujishughulisha na mambo ya dunia hii, jinsi atakavyompendeza mkewe.
34 Tena iko tofauti hii kati ya mke na mwanamwali. Yeye asiyeolewa hujishughulisha na mambo ya Bwana, apate kuwa mtakatifu mwili na roho. Lakini yeye aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia hii, jinsi atakavyompendeza mumewe.
35 Nasema hayo niwafaidie, si kwamba niwategee tanzi, bali kwa ajili ya vile vipendezavyo, tena mpate kumhudumia Bwana pasipo kuvutwa na mambo mengine.
36 Lakini mtu awaye yote akiona ya kuwa hamtendei mwanamwali wake ipendezavyo, na ikiwa huyo amepita uzuri wa ujana wake, na ikiwapo haja, basi, afanye apendavyo, hatendi dhambi, na awaruhusu waoane.
37 Lakini yeye aliyesimama kwa uthabiti wa moyo wake, hana sharti, lakini aweza kuyatawala mapenzi yake, tena amekusudia moyoni mwake kumlinda mwanamwali wake, atatenda vema.
38 Basi, hivyo na amwozaye mwanamwali wake afanya vema; na yeye asiyemwoza atazidi kufanya vema.
39 Mwanamke hufungwa maadamu mumewe yuko hai, lakini ikiwa mumewe amefariki, yuko huru kuolewa na mtu yeyote amtakaye; katika Bwana tu.
40 Lakini heri yeye zaidi akikaa kama alivyo; ndivyo nionavyo mimi, nami nadhani ya kuwa mimi nami nina Roho wa Mungu.
2 Wakorintho 6 : 14
14 ⑭ Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?
Mwanzo 2 : 24
24 ⑤ Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.
1 Wakorintho 6 : 19 – 20
19 ⑲ Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe;
20 ⑳ maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu.
Warumi 1 : 26 – 27
26 Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili;
27 wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao.
Mathayo 19 : 1 – 30
1 ⑭ Ikawa Yesu alipomaliza maneno hayo, akatoka Galilaya akafika katika eneo la Yudea, ng’ambo ya Yordani.⑮
2 Makutano mengi wakamfuata, akawaponya huko.
3 ⑯ Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamjaribu, wakimwambia, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe kwa sababu yoyote?
4 ⑰ Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mwanamume na mwanamke,
5 ⑱ akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja?
6 ⑲ Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.
7 ⑳ Wakamwambia, Jinsi gani basi Musa aliamuru kumpa hati ya talaka, na kumwacha?
8 Akawaambia, Musa, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi.
9 Nami nawaambia ninyi, Kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini.
10 Wanafunzi wake wakamwambia, Mambo ya mtu na mkewe yakiwa hivyo, haifai kuoa.
11 Lakini yeye akawaambia, Si wote wawezao kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwa.
12 Maana wako matowashi waliozaliwa hali hiyo toka matumboni mwa mama zao; tena wako matowashi waliofanywa na watu kuwa matowashi; tena wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea neno hili, na alipokee.
13 Ndipo akaletewa watoto wadogo ili aweke mikono yake juu yao na kuwaombea; wanafunzi wake wakawakemea.
14 Lakini Yesu akasema, Waacheni watoto wadogo waje kwangu; wala msiwazuie; kwa maana walio mfano wa hao, ufalme wa mbinguni ni wao.
15 Akaweka mikono yake juu yao, akatoka huko.
16 Na tazama, mtu mmoja akamwendea akamwambia, Mwalimu, nitende jambo gani jema, ili nipate uzima wa milele?
17 Akamwambia, Kwa nini uniulize kuhusu wema? Aliye mwema ni mmoja. Lakini ukitaka kuingia katika uzima, zishike amri.
18 Akamwambia, Zipi? Yesu akasema, Ni hizi, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo,
19 Waheshimu baba yako na mama yako, na, Mpende jirani yako kama nafsi yako.
20 Yule kijana akamwambia, Haya yote nimeyashika; nimepungukiwa na nini tena?
21 Yesu akamwambia, Ukitaka kuwa mkamilifu, nenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.
22 Yule kijana alipolisikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.
23 Yesu akawaambia wanafunzi wake, Amin, nawaambieni, ya kwamba itakuwa shida tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni.
24 Nawaambia tena, Ni rahisi zaidi ngamia kupenya tundu ya sindano, kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.
25 Wanafunzi waliposikia, walishangaa mno, wakisema, Ni nani basi awezaye kuokoka?
26 Yesu akawakazia macho, akawaambia, Kwa wanadamu hilo haliwezekani; bali kwa Mungu yote yawezekana.
27 Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?
28 Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.
29 Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele.
30 Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.
Leave a Reply