Hizi ndizo Aya za Biblia zinazozungumzia mume
Waefeso 5 : 25 – 33
25 Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda kanisa, akajitoa kwa ajili yake;
26 ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno;
27 apate kujiletea kanisa tukufu, lisilo na dosari wala kunyanzi wala lolote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa.
28 Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe.
29 Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake popote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea kanisa.
30 Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake.
31 Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja.
32 Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na kanisa.
33 Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe.
1 Wakorintho 7 : 1 – 7
1 Basi kuhusu mambo yale mliyoandika, ni heri mwanamume asimguse mwanamke.
2 Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe.
3 Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake.
4 Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe.
5 Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkarudiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu.
6 Lakini nasema hayo, kwa kutoa idhini yangu, si kwa amri.
7 Ila nipendalo ni kwamba watu wote wawe kama mimi nilivyo; lakini kila mtu ana karama yake mwenyewe itokayo kwa Mungu, huyu hivi, na huyu hivi.
1 Petro 3 : 1 – 22
1 Kadhalika ninyi wake, watiini waume zenu; kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile Neno;
2 wakiutazama mwenendo wenu safi, na wa hofu.
3 Kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi;
4 bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu.
5 Maana hivyo ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu, na kuwatii waume zao.
6 Kama vile Sara alivyomtii Abrahamu, akamwita bwana; nanyi ni watoto wake, mfanyapo mema, pasipo kutishwa na hofu yoyote.
7 Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; maana wao pia ni warithi wa neema ya uzima, ili maombi yenu yasizuiliwe na chochote.
8 Neno la mwisho ni hili; muwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikitikivu, wanyenyekevu;
9 watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi baraka.
10 Kwa maana, Atakaye kupenda maisha, Na kuona siku njema, Auzuie ulimi wake usinene mabaya, Na midomo yake isiseme uongo.
11 Na aache mabaya, atende mema; Atafute amani, aifuate sana.
12 Kwa kuwa macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake husikiliza maombi yao; Bali uso wa Bwana uko juu ya watenda mabaya.
13 Naye ni nani atakayewadhuru, mkiwa wenye juhudi katika mema?
14 Lakini hata mkiteswa kwa sababu ya kutenda haki, mna heri. Msiogope kutisha kwao, wala msifadhaike; bali mtakaseni Kristo Bwana mioyoni mwenu.
15 Muwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa heshima.
16 Nanyi muwe na dhamiri njema, ili katika neno lile mnalosingiziwa, watahayarishwe wale wautukanao mwenendo wenu mwema katika Kristo.
17 Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya.
18 Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; akauawa kimwili, lakini akahuishwa kiroho,
19 ambayo kwa hiyo aliwaendea roho waliokaa kifungoni, akawahubiria;
20 watu wasiotii hapo zamani, wakati Mungu alipowavumilia kwa subira, siku za Nuhu, safina ilipokuwa ikitengenezwa; ambamo ndani yake wachache, yaani, watu wanane, waliokoka kwa maji.
21 Mfano wa mambo hayo ni ubatizo, unaowaokoa ninyi pia siku hizi; (siyo kuwekea mbali uchafu wa mwili, bali jibu la dhamiri safi mbele za Mungu), kwa kufufuka kwake Yesu Kristo.
22 Naye yuko katika mkono wa kulia wa Mungu, amekwenda zake mbinguni, malaika na enzi na nguvu zikiisha kutiishwa chini yake.
1 Wakorintho 7 : 10 – 11
10 Lakini wale waliokwisha kuoana nawaagiza; wala hapo si mimi, ila Bwana; mke asiachane na mumewe;
11 lakini, ikiwa ameachana naye, na akae asiolewe, au apatane na mumewe; tena mume asimwache mkewe.
Leave a Reply