Hizi ndizo Aya za Biblia zinazozungumzia israel na Palestina
Amosi 9 : 7
7 ③ Je! Ninyi si kama wana wa Wakushi kwangu mimi, enyi wana wa Israeli, asema BWANA? Je! Mimi sikuwapandisha Israeli toka nchi ya Misri, na Wafilisti toka Kaftori, na Washami toka Kiri?
Yoshua 1 : 2 – 3
2 Musa mtumishi wangu amefariki; sasa ondoka, vuka mto huu wa Yordani; wewe na watu hawa wote, mkaende hadi nchi niwapayo wana wa Israeli.
3 Kila mahali zitakapopakanyaga nyayo za miguu yenu, nimewapa ninyi, kama nilivyomwapia Musa.
Mwanzo 15 : 18
18 Siku ile BWANA akafanya agano na Abramu, akasema, Uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Frati,
Mathayo 24 : 1 – 51
1 Yesu akaenda zake, akatoka hekaluni; wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonesha majengo ya hekalu.
2 Naye akajibu akawaambia, Hamyaoni haya yote? Amin, nawaambieni, Halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomolewa.
3 Hata alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamwendea kwa faragha, wakisema, Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia?
4 Yesu akajibu, akawaambia, Angalieni, mtu asiwadanganye.
5 Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi.
6 Nanyi mtasikia habari za vita na tetesi za vita; angalieni, msitishwe; maana hayo hayana budi kutukia; lakini ule mwisho bado.
7 Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na njaa, na mitetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali.
8 Hayo yote ndiyo mwanzo wa uchungu.
9 Wakati huo watawasaliti ninyi mpate dhiki, nao watawaua; nanyi mtakuwa watu wa kuchukiwa na mataifa yote kwa ajili ya jina langu.
10 Ndipo wengi watakapojikwaa, nao watasalitiana, na kuchukiana.
11 Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi.
12 Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapunguka.
13 Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka.
14 Tena Habari Njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.
15 Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu),
16 ndipo walio katika Yudea na wakimbilie milimani;
17 naye aliye juu ya dari asishuke kuvichukua vitu vilivyomo nyumbani mwake;
18 wala aliye shambani asirudi nyuma kuichukua nguo yake.
19 Ole wao wenye mimba na wanyonyeshao siku hizo!
20 Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato.
21 Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe.
22 Na kama siku hizo zisingalifupishwa, asingeokoka mtu yeyote; lakini kwa ajili ya wateule siku hizo zitafupishwa.
23 Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki.
24 Kwa maana watatokea Makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, ikiwezekana, hata walio wateule.
25 Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele.
26 Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki.
27 Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.
28 Kwa kuwa popote ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai.
29 Lakini mara tu, baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka kutoka mbinguni, na nguvu za mbinguni zitatikisika;
30 ① ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi.
31 ② Naye atawatuma malaika wake pamoja na sauti kuu ya parapanda, nao watawakusanya wateule wake toka pepo nne, toka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho huu.
32 Basi kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mnatambua ya kuwa wakati wa mavuno uko karibu;
33 nanyi kadhalika, myaonapo mambo hayo yote, tambueni ya kuwa yuko karibu, katika malango.
34 Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia.
35 ③ Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
36 ④ Lakini kuhusu siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake.
37 ⑤ Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.
38 ⑥ Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hadi siku ile aliyoingia Nuhu katika safina,
39 ⑦ wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.
40 ⑧ Wakati ule watu wawili watakuwako shambani; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa;
41 wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.
42 ⑩ Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu.
43 ⑪ Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliujua ule wakati mwizi atakaokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa.
44 ⑫ Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyotazamia Mwana wa Adamu yuaja.
45 Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake?
46 Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo.
47 ⑬ Amin, nawaambieni, atamweka juu ya vitu vyake vyote.
48 ⑭ Lakini mtumwa yule mbaya akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia;
49 akaanza kuwapiga watumwa wenzake, na kula na kunywa pamoja na walevi;
50 bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyotazamia, na saa asiyojua,
51 ⑮ atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wanafiki; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.
1 Petro 1 : 1 – 25
1 Petro, mtume wa Yesu Kristo, kwa wateule wa Utawanyiko, wakaao hali ya ugeni katika Ponto, na Galatia, na Kapadokia, na Asia, na Bithinia;
2 kama vile Mungu Baba alivyotangulia kuwajua katika kutakaswa na Roho, hata mkapata kutii na kunyunyiziwa damu ya Yesu Kristo. Neema na amani na ziongezwe kwenu.
3 Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu;
4 tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu.
5 Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani ili mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho.
6 Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa muda mfupi, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali;
7 ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo.
8 Naye mwampenda, ijapokuwa hamkumwona; ambaye ijapokuwa hamumwoni sasa, mnamwamini; na kufurahi sana, kwa furaha isiyoneneka, yenye utukufu,
9 katika kuupokea mwisho wa imani yenu, yaani, wokovu wa roho zenu.
10 Kuhusu wokovu huo, manabii ambao walitabiri habari za neema itakayowafikia ninyi, walichunguza sana.
11 Wakatafuta ni wakati upi, na wakati wa namna gani ulioonywa na Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, ambaye alitangulia kuyashuhudia mateso yatakayompata Kristo, na utukufu utakaokuwako baada ya hayo.
12 Wakafunuliwa ya kuwa si kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yenu walihudumu katika mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiria ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Mambo hayo malaika wanatamani kuyaona.
13 Kwa hiyo iweni tayari, na makini;[1] mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu Kristo.
14 Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu;
15 bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;
16 kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.
17 Na ikiwa mnamwita Baba, yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake, nendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni.
18 Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu;
19 bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na dosari wala waa, yaani, ya Kristo.
20 Naye amejulikana kweli tangu zamani, kabla haijawekwa misingi ya dunia; lakini alifunuliwa siku hizi za mwisho kwa ajili yenu;
21 na kupitia kwake mmekuwa wenye kumwamini Mungu, aliyemfufua katika wafu akampa utukufu; hata imani yenu na tumaini lenu liwe kwa Mungu.
22 Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii kweli, hata kuufikia upendano wa ndugu usio na unafiki, basi jitahidini kupendana kwa moyo safi.
23 Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu lenye uzima, linalodumu hata milele.
24 Maana, Mwili wote ni kama majani, Na fahari yake yote ni kama ua la majani. Majani hukauka na ua lake huanguka;
25 Bali Neno la Bwana hudumu hata milele. Na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.
Leave a Reply